Kuna ujumbe mmoja muhimu sana ambao ningependa kuwashirikisha katika Siku ya Dunia ya mwaka 2025: Nawasihi wote tuitendee kila siku ya mwaka kama Siku ya Dunia. Sayari Dunia ndiyo nyumba pekee tunayofahamu, lakini tunaendelea kuidhuru kwa kasi isiyo na huruma. Tunaharibu misitu, maeneo ya miti, maeneo oevu, ardhi za mabanio, savanna, majani marefu na mifumo mingine yote ya kiikolojia ambayo sijaitaja. Tunasababisha uchafuzi wa mito, maziwa na bahari. Tunatoa gesi chafu zinazoongeza joto duniani, hali inayosababisha mabadiliko ya hali ya hewa kama vile vimbunga, tufani, mafuriko, ukame, mawimbi ya joto na moto wa misitu unaoweza kuharibu nyumba zetu. Tuko katikati ya kutoweka kwa wingi kwa mimea na wanyama – ya sita katika historia ya dunia.
Tukiongeza kwenye orodha hii ukweli kwamba mamia ya maelfu ya watu wanateseka kwa sababu ya vita, umasikini na ubaguzi – basi si ajabu kuwa watu wengi zaidi wanapoteza matumaini. Watu huuliza kama bado nina matumaini kuhusu mustakabali wetu. Naam, naamini kuwa bado kuna dirisha la muda ambapo tunaweza angalau kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bioanuwai. Lakini ni kwa masharti ya kushirikiana na kuchukua hatua sasa. Bila matumaini, tutakumbwa na hali ya kutofanya chochote – na basi tutakuwa tumeangamia.
Hebu niwashirikishe sababu zangu za kuwa na matumaini – na nafikiri wengi wenu mnazifahamu tayari.
Kwanza kabisa, ni vijana wetu. Kila mahali duniani, mara tu wanapofahamu matatizo na kupewa nguvu ya kuchukua hatua, wanainuka na kukabiliana nayo. Harakati yetu ya R&S, ambayo sasa ipo katika nchi 75, inakua kwa kasi, na inahusisha vijana wa rika zote. Wanabadilisha mambo kwa kweli, mara nyingi wakiwa na ushawishi kwa wazazi wao, babu na bibi zao, walimu na marafiki.
Pili, asili ina uwezo mkubwa wa kupona – nimeona maeneo mengi yaliyoharibiwa kabisa yakianza kurejea katika hali yake ya awali pindi yanapopewa muda, na wakati mwingine msaada (mara nyingi kutoka kwa R&S). Niliandika kitabu kuhusu wanyama waliokuwa karibu kutoweka lakini wakapewa nafasi nyingine ya kuishi – kwa sababu ya watu binafsi waliodhamiria wasiishe. Watu wanaoonesha roho ile isiyokata tamaa ya kibinadamu, wakikabili mambo yaliyoonekana hayawezekani na kufanikiwa. Na pia kuna akili yetu ya kipekee kama binadamu. Wanasayansi wanafanya kazi kutengeneza teknolojia zitakazotuwezesha kuishi kwa usawa zaidi na mazingira, kama vile nishati mbadala.
Labda unajiuliza, jambo hili linanihusu vipi? Naweza kufanya nini kuhusu haya yote? Nakwambia kuwa kila siku unayoishi unafanya athari fulani duniani – na unaweza kuchagua ni athari ya aina gani utafanya. Unaweza kukumbuka kuzima taa. Labda unaweza kutembea kwa miguu, kutumia baiskeli, treni au basi badala ya gari. Unaweza kufikiria kuhusu kile unachonunua – je, kilisababisha madhara kwa mazingira? Je, kilisababisha mateso kwa wanyama? Je, ni cha bei rahisi kwa sababu wafanyakazi walilipwa ujira mdogo? Kisha tafuta bidhaa iliyo na maadili zaidi. Je, itagharimu zaidi? Huenda, lakini utaithamini zaidi na kupunguza upotevu. Na upotevu ni tatizo kubwa sana kwa sasa.
Jambo jingine muhimu sana unaloweza kufanya ni kuanza kula mlo wa mimea. Kwa sehemu kwa sababu itapunguza sana mateso ya mabilioni ya wanyama wanaofungiwa kwenye mashamba ya viwandani, na pia kwa sababu maeneo makubwa ya makazi ya asili hufyekwa ili kulima chakula cha kuwalisha wanyama hao. Maji mengi yanahitajika kubadilisha protini ya mboga kuwa protini ya mnyama, na wanyama hutoa gesi ya methani wakati wa mmeng’enyo wa chakula – gesi hatari sana ya hewa ukaa. Na ni muhimu kusema kuwa ni njia bora kiafya kwetu binadamu pia.
Mamilioni, na hatimaye mabilioni ya watu wakianza kufikiria kuhusu athari zao kwa mazingira, italeta mabadiliko makubwa na kusaidia kuponya Mama Dunia. Na kumbuka, tunategemea dunia ya asili kwa chakula, maji – kwa kweli kila kitu. Kwa hiyo, kwa ajili ya watoto wetu na vizazi vyote vijavyo, tafadhali anza leo, si tu katika Siku hii ya Dunia ya mwaka 2025, bali katika kila siku zinazokuja.
Asanteni sana.
Dkt. Jane Goodall, DBE
Mwanzilishi – Taasisi ya Jane Goodall
Na Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa
Tagi: Habari ya Kwanza