Kiwanda cha Asali cha Tanzania Kuanza Kusafirisha Bidhaa Marekani Kupitia Ushirikiano wa USAID-JGI

Kategoria: Kategoria ya Kwanza
Imechapishwa: 2024-12-16 09:28:16

Kigoma – Marekani, kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), inashirikiana na Taasisi ya Jane Goodall (JGI), Upendo Honey, na kampuni ya kijamii ya Marekani, Burlap & Barrel, kusafirisha asali inayovunwa Tanzania kwa walaji wa Marekani. Hivi karibuni, walaji wa Marekani wataweza kununua asali hii ya asili ya Tanzania mtandaoni na kuipata moja kwa moja majumbani mwao.

Moyo wa mradi huu ni uzalishaji wa asali bora, iliyothibitishwa kuwa ya asili—bidhaa inayoweza kuvunwa tu kutoka kwenye misitu iliyo mbali na kilimo, ufugaji, na makazi ya binadamu. Mbinu hii inasaidia kulinda misitu isiyoathiriwa, kama vile misitu ya Miombo ya Tanzania, huku ikiruhusu jamii kupata hadi mara tatu ya bei ya kawaida ya soko kwa ajili ya asali yao. Ushirikiano huu unabadilisha ufugaji nyuki wa kienyeji kuwa chanzo endelevu cha uchumi huku ukilinda makazi muhimu ya wanyamapori, wakiwemo sokwe waliomchochea Dkt. Jane Goodall kufanya utafiti wake wa kipekee katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Tanzania.

"Asali hii siyo tu kwamba ni tamu—ina badilisha maisha," alisema Dkt. Goodall. "Uvunaji na uuzaji wa asali hii hutoa kipato kinachohitajika sana kwa familia za Kitanzania huku ikihifadhi mifumo muhimu ya ikolojia inayosaidia watu na wanyamapori."

Mpango huu unawawezesha wazalishaji wa asali wa Tanzania kwa kuwaunganisha na masoko ya Marekani na ya kimataifa, na hivyo kuleta fursa mpya za ukuaji na ustawi. Wakati huohuo, mradi huu unachochea juhudi za jamii kulinda na kurejesha bioanuwai huko Magharibi mwa Tanzania. Ushirikiano huu unawezekana kwa msaada wa USAID Hope Through Action, mradi mkuu wa USAID unaozingatia kuweka jamii katikati ya uhifadhi, kukuza maendeleo endelevu, na kuimarisha mustakabali mzuri kwa watu na mazingira. Hivi sasa, karibu wafugaji nyuki 1,100 wanaoshiriki katika mradi wa USAID Hope Through Action wanashiriki katika mpango wa asali ya asili, wakizalisha karibu tani 150 za asali kila mwaka.

"Msaada wa USAID umekuwa muhimu katika kufanya maono haya kuwa halisi," alisema Craig Hart, Mkurugenzi wa USAID/Tanzania. "Ushirikiano huu kati ya Burlap & Barrel, Taasisi ya Jane Goodall, na Upendo Honey ya Tanzania unaonyesha nguvu ya kuwaunganisha jamii za ndani na masoko ya kimataifa ili kufanikisha manufaa ya kudumu kwa bioanuwai na maisha ya watu."

Mbali na kuongeza mapato ya ndani, asilimia tano ya bei ya rejareja ya kila chupa ya asali itachangwa kwa kazi za uhifadhi za JGI Magharibi mwa Tanzania, kuhakikisha mustakabali wa kijani, endelevu, na uliojaa matumaini kwa watu na wanyamapori kwa pamoja.

Kwa maelezo zaidi kuhusu taarifa hii ya vyombo vya habari, tafadhali wasiliana na timu ya Maendeleo, Uhamasishaji na Mawasiliano ya USAID/Tanzania kupitia Dardocs@usaid.gov.

 

Chanzo: https://www.usaid.gov/tanzania/press-release/dec-13-2024-tanzanian-honey-factory-begins-exports-us-through-usaid-jgi-partnership

Tagi: Habari ya Kwanza